Colossians 3

Kanuni Za Kuishi Maisha Matakatifu

1 aBasi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Al-Masihi, yatafuteni yaliyo juu, Al-Masihi alikoketi mkono wa kuume wa Mungu. 2 bYafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani. 3 cKwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Al-Masihi katika Mungu. 4 dWakati Al-Masihi, aliye uzima wenu, atakapotokea, ndipo nanyi mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.

5 eKwa hiyo, ueni kabisa chochote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: yaani uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na ulafi, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. 6 fKwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja. 7 gNinyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo. 8 hLakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote: yaani hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu. 9 iMsiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10 jnanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11 kHapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Al-Masihi ni yote, na ndani ya wote.

12 lKwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 mVumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 nZaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

15 oAmani ya Al-Masihi na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 pNeno la Al-Masihi na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 qLolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Isa, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

Kanuni Katika Madaraka Ya Nyumbani

18Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana.

19 rNinyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu dhidi yao.

20 sEnyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana.

21 tNinyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

22 uNinyi watumwa, watiini mabwana zenu wa hapa duniani katika mambo yote. Fanyeni hivyo si wakiwepo tu, wala si kwa kutafuta upendeleo wao, bali kwa moyo mnyofu na kumcha Bwana. 23 vLolote mfanyalo, fanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana, na si wanadamu, 24 wkwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana ukiwa thawabu yenu. Ni Bwana Isa Al-Masihi mnayemtumikia. 25 xYeyote atendaye mabaya atalipwa kwa ajili ya mabaya yake, wala hakuna upendeleo.
Copyright information for SwhKC